Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Mhe Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara anayoisimamia ipo tayari kutoa mashirikiano yoyote yanayohitajika kwa Taasisi ya Mpango wa hiyari wa nchi za Umoja wa Afrika kujitathmini katika vigezo vya Utawala Bora (APRM Tanzania).

Hayo ameyabainisha katika kikao kazi, kilichofanyika katika Ofisi ya Mhe Haroun wakati uongozi wa APRM Tanzania ulipofika katika Ofisi yake kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kupanga mikakati bora ya kuimarisha mahusiano ili kwa pamoja waweze kufanikisha Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Tanzania.

Mhe Haroun amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa Utawala Bora na ndio mana inachukua hatua mbali mbali za kuuimarisha ikiwa ni pamoja na kuwepo Idara maalum inayohusika na masuala ya utawala Bora, haki za binadamu, lakini pia kuwasilishwa kwa uwazi Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali  jambo ambalo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi  ameahidi kuwa litakuwa ni endelevu.

Ameongeza kuwa wizara anayoisimamia ina ukaribu na mashirikiano makubwa na APRM tokea kuanzishwa kwake, na ameishukuru sana kwa kuwapatia mialiko mbali mbali watendaji wake na amewaomba kudumisha mahusiano hayo kwa kuhakikisha kuwa fursa zinazopatikana pia ziweze kuwafikia watendaji wa Ofisi hiyo ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mikutano na mafunzo mbali mbali ndani na nje ya Tanzania.

Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Ndg Mansoura Kassim amesema kuwa APRM inapaswa kufanya kazi kwa ukaribu mkubwa na Idara ya Utawala Bora Zanzibar ambayo pia inafanya tathmini mbali mbali za ndani pamoja na kuweza kusaidia juu ya upatikanaji wa nyaraka zinazohusiana na masuala ya Utawala Bora Zanzibar.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Ndg Lamau Mpolo amesema kuwa mashirikiano wanayoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mazuri na ya kupigiwa mfano, jambo ambalo litapelekea taarifa za Zanzibar kuhusiana na masuala ya Utawala Bora kuonekana kwa vizuri Zaidi katika Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora.

Ameongeza kuwa, Ripoti za APRM zinalenga kukuza dhana ya Utawala Bora kwa kutekeleza sera, viwango na Taratibu zitakazopelekea kuimarika kwa siasa,kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi,uhakika wa maendeleo endelevu pamoja na kuharakisha mtangamano wa kikanda na Bara zima la Afrika kwa kuibua changamoto zilizopo kuziandalia mpango kazi wa kuzitatua.

Mkurugenzi Idara ya Ubora Zanzibar Bi Zaina Daud Khalid amewasisitiza uongozi wa APRM kuhakikisha kuwa wanaimarisha mawasiliano na watendaji wa Idara ya Utawala Bora pamoja na Taasisi nyengine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na wanapohitaji taarifa au nyaraka zozote watoe taarifa mapema ili ziweze kuandaliwa na kufanikisha maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Tanzania.