Katibu Mtendaji wa Mpango wa Hiari wa kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania (APRM) Bw Lamau Mpolo amesema kuwa Tanzania imepokea ugeni kutoka makao makuu ya APRM Afrika kusini kwa lengo la kufuatilia maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala bora nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo katika kikao kilichofanyika baina ya uongozi wa APRM Tanzania na baadhi ya viongozi kutoka makao makuu ya APRM Afrika Kusini, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar-es-salaam.

Katibu Mtendaji Mpolo amesema kuwa ugeni huo unatarajiwa kuwepo Tanzania kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 01/08/2023 hadi tarehe 05/8/2023 kwa lengo la kutoa miongozo na ushirikiano katika kuelekea Tathmini ya Ripoti ya Pili ya Utawala Bora Tanzania.

Ameongeza kuwa katika ugeni huo, ambao pia unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa kubadilishana uzoefu katika mikutano miwili inayotarajia kufanyika tarehe 03/08/2023 na tarehe 05/08/2023 kuhusu masuala ya ‘Credit Rating’ pamoja na maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala bora.

Akiongea katika mkutano huo, Mkurugenzi Muendeshaji wa APRM Makao Makuu Bw Ferdinand Katendeko amesema kuwa ujio wao Tanzania una lengo zuri la kuhakikisha kuwa Tanzania inafanikiwa kuandaa Ripoti ya Pili ya Utawala Bora kwa kuzingatia misingi ya APRM ikiwemo suala la ushirikishwaji kwa wadau.

Amesisitiza kuwa Tanzania ina mambo mengi makubwa na mazuri ya kujivunia kuhusu Utawala Bora ikiwemo Muungano wa Tanzania uliodumu kwa muda mrefu, matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili na mengine mengi mazuri na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kwa uwazi kwa kuangalia maeneo ambayo yana changamoto ili Serikali iweze kuyatambua na  kuyafanyia kazi.