SUZA na APRM kushirikiana katika Tafiti za Utawala Bora

Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya  Mpango wa Hiari wa Kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora(APRM Tanzania), kwa lengo la kuimarisha tafiti zinazolenga kukuza utawala bora nchini Tanzania. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ofisi za Chuo hicho Tunguu Zanzibar, ambapo SUZA ilieleza dhamira yake ya kutumia wataalamu wake kuhakikisha tafiti zinaendana na mahitaji halisi ya jamii na mipango ya kitaifa.

Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Mohammed Makame Haji, alisema chuo hicho kina hazina kubwa ya wataalamu waliobobea katika nyanja mbalimbali ambao wanaweza kusaidia katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya taifa. Alisisitiza kuwa tafiti hizo zitazingatia soko la ajira, ustawi wa mwananchi wa kawaida na kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Prof. Haji alibainisha kuwa elimu na tafiti ni nyenzo muhimu katika kufanikisha dira hiyo, na kuongeza kuwa SUZA itaendelea kupanua wigo wake wa ushirikiano ili kuhakikisha inatoa mchango mkubwa si tu kwa Tanzania bali hata kwa bara la Afrika kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bw. Lamau Mpolo, amesema kuwa APRM imejipanga kuhamasisha utawala bora kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu kama SUZA, ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zina tija na zinajikita kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa wa kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa SUZA imejijengea heshima kubwa nchini na kwamba ushirikiano huo utaleta matokeo chanya katika kuendeleza jitihada za maendeleo, huku akiitaka SUZA kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa APRM katika shughuli zake.

Aidha, Bwana Mpolo aliupongeza uongozi wa SUZA kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha, hususan katika mchakato wa maandalizi ya kitabu kinachoakisi mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya awamu ya Nane ya  Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Alisema uongozi wa SUZA umeonesha dhamira ya kweli na mshikamano wa hali ya juu bila kuweka vikwazo, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa taifa.

Itakumbukwa kuwa, utiaji saini wa mkataba huo wa mashirikiano umekuja kufuatia kikao kilichofanyika tarehe 27 Machi 2025 katika ofisi za SUZA Tunguu, Zanzibar, ambacho kilijadili kwa kina namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika sekta ya tafiti, elimu na utawala bora.