Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia kwa vitendo kufanya Tathmini ya Pili katika masuala ya Utawala Bora Nchini na jambo hilo limekuja wakati muafaka kwa Tanzania kwavile inafanya vizuri katika masuala mbali mbali ya Kidemokrasia na huduma za kijamii.

Hayo yamedhihirishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe George Simbachawene wakati akizungumza na ujumbe wa APRM ngazi ya Bara uliongozwa na Prof Eddy Maloka, mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ya Utumishi Dar-es-Salaam, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe Simbachawene amesema kuwa Mhe Rais ameridhia kwa vitendo kufanikisha Ripoti ya pili ya Tathmini ya Utawala bora kwa vile Tanzania inajivunia mabadiliko makubwa yaliyofanyika ambayo yanatokana na Ripoti ya kwanza ya tathmini ya Utawala bora hivyo serikali imejidhatiti kufanikisha hilo ili ulimwengu uweze kutambua mazuri ya Tanzania na kwa namna gani ilivyoimarika katika masuala ya utawala bora.
Aidha amemshukuru Mtendaji Mkuu wa APRM ngazi ya Bara Prof Eddy Maloka Pamoja na ujumbe wake kwa ziara yao Tanzania na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuwaunga mkono kutokana na umuhimu mkubwa wa chombo cha APRM kwa Serikali lakini pia kwa wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Prof Eddy Maloka ambae ni Mtendaji Mkuu wa APRM makao Makuu Afrika Kusini amesema kuwa amefurahishwa sana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwamuzi wake wa busara wa kuamua kuajiri watendaji wapya ambao watahakikisha APRM Tanzania inasimama na kufanikisha Ripoti hiyo lakini pia kuwapangia bajeti kubwa ambayo itahakikisha shughuli za APRM zinaendelea kwa ufanisi mkubwa.

Aidha ameongeza kuwa APRM Makao Makuu itatoa kila aina ya ushirikiano kwa Tanzania Pamoja na kutengeneza mpango kazi wa Pamoja na bajeti ili kuhakikisha kuwa Ripoti ya pili ya Tathmini inafanyika na kumalizika kwa muda ambao umepangwa.

Ameongeza kuwa wakati APRM inaelekea kusherehekea miaka 20 tokea kuanzishwa kwake Tanzania itashiriki katika Sherehe hizo ili nchi wanachama waweze kukutana kwa Pamoja na kubadilishana uzoefu, pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono mpango huu wa hiyari wa Nchi za Umoja wa Afrika katika kujitathmini kiutawala Bora.