Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati kusimamia na kuendeleza masuala ya Utawala Bora Nchini na tayari imejipanga na kukubali kuandaa Ripoti ya Pili ya Tathmini ya masuala ya Utawala Bora Nchini.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) wakati alipokutana na ujumbe kutoka APRM ngazi ya Bara uliongozwa na mtendaji mkuu Prof Eddy Maloka katika Ofisi za Wizara Jijini Dar-es-salaam.
Mhe Tax amesema kuwa Ripoti ya kwanza ya masuala ya utawala bora nchini iliiletea sifa kubwa Tanzania hivyo awamu hii ya pili Serikali imeamua kuongeza nguvu kwa kuajiri watendaji wapya Pamoja na kuhakikisha kuwa ufanisi mkubwa unapatikana kuanzia maandalizi hadi kutoka kwa Ripoti hiyo.
Aidha amemshukuru sana Prof Maloka na ujumbe wake kwa maamuzi yao ya kuja Tanzania kukutana na viongozi wa Serikali Pamoja na watendaji wa APRM na kumuomba kuendelea kuwaunga mkono katika kuhakikisha APRM inasimama na kufanikisha Ripoti hiyo ya Pili.
Akizungumza katika mkutano huo Prof Eddy Maloka amesema kuwa ujio wao huo umelenga Zaidi kuonana na uongozi mpya wa APRM Tanzania ambapo wana Imani kubwa watafanya vizuri lakini pia ameahidi kutoa mashirikiano katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa kinara na kuandaa Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora kwa ufanisi mkubwa.
Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Balozi Fatma M. Rajab amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa chombo cha APRM Tanzania kwani kinawezesha wadau kutoa maoni yao ambayo yataisaidia Serikali kurekebisha pale penye mapungufu.
Ameongeza kuwa kupitia Ripoti ya kwanza mambo mengi sana yamebadilika, hivyo Serikali imefaya maamuzi ya kishujaa kufanya Tathmini ya Pili ili kujitambua na kuongeza nguvu katika yale maeneo ambayo yanafanya vizuri.








