Msisitizo wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni Diplomasia ya Uchumi. Ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako kuwa, Wizara imekamilisha rasimu ya awali ya Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. Mkakati huu umeianisha maeneo saba ya kipaumbele ambayo Wizara itayatilia mkazo katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Maeneo hayo ni pamoja na;
(i) Kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje
(ii) Kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi
(iii) ​Kuvutia watalii kuja Tanzania
(iv) ​Kutafuta misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje
(v) ​Kutafuta fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi
(vi) ​Kujenga taswira nzuri ya nchi yetu kimataifa
(vii) ​Kujenga uwezo wa kitaasisi wa Wizara, na Wizara na Taasisi nyingine kusimamia vizuri utekelezaji wa Mkakati wa Diplomasia ya Uchumi.