Wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia wameombwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Mpango wa hiyari ya kujitathmini kiutawala Bora (APRM Tanzania) kwa kuwa Mabalozi wazuri wa kueneza taaluma walioipata kuhusu dhana ya APRM
Hayo yamesemwa na Muheshimiwa Balozi Hemedi Mgaza wakati akiwasilisha mada kuhusu APRM Tanzania na majukumu yake katika mafunzo mafupi yaliotolewa na APRM yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo hicho Kurasini Jijini Dar-es- Salaam.
Balozi Mgaza amesema kuwa ni vyema kuifahamu kwa undani APRM na majukumu yake kwavile ndio mdomo wa wananchi kuitathimini Serikali yao hivyo APRM imejipanga kutoa taaluma hiyo kwa makundi mbalimbali Tanzania ili elimu hiyo iweze kufika mbali na kumfikia kila mwananchi.
Ameongeza kuwa APRM Tanzania ipo katika maandalizi ya kuandaa Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora ambapo kila mwananchi kwa nafasi yake anapaswa ashiriki ili Serikali itambue mazuri yake iweze kuyaendeleza lakini pia ijue wapi kuna changamoto wazitatue na wananchi waweze kupata maendeleo.
Kwa upande wake Meneja Habari na Mawasiliano Badria Masoud amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imeupa nguvu sana mpango huu wa Tathmini, hivyo ni vyema kwa wananchi kuwa tayari kuelezea kwa undani masuala ya utawala bora kwavile Ripoti itakayoandikwa itawasilishwa mbele ya Marais wa Nchi 42 za Afrika walioridhia mpango huu.
Badria amesisitiza kuwa Serikali inaitegemea sana Ripoti ambayo itaandaliwa na APRM Tanzania ambayo itakuwa na mawazo halisi ya wananchi ili iweze kujipima katika vigezo vya utawala bora.
Kwa upande wake Raisi wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Cha Diplomasia Muheshimiwa Joshua Godfrey kwa niaba ya wanafunzi amesema kuwa ujio wa APRM umewafurahisha sana na unaonesha kiasi gani wana thamani kwa APRM, hivyo ameahidi kuwa watakuwa mabalozi wazuri kuhakikisha kuwa elimu walioipata wanaifanyia kazi na kuifikisha kwa wadau wengine.











