Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amefungua Mkutano wa Nne wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara unaofanyika jijini Arusha.

Akifungua Mkutano huo, Mhe. Balozi Mbarouk amewasihi Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kubuni maeneo ya kimkakati ya ushirikiano ambayo yatakuza na kuendeleza ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya Kikanda na Kimataifa.

“Nichukue fursa hii kuwasihi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ubunifu, muendelee kubuni maeneo ya kimkakati ya ushirikiano ili kuimarisha uhusiano wa uwili, kikanda na Kimataifa kuendeleza ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa,” alisisitiza Balozi Mbarouk.

Amesema Wizara inaandelea na kazi ya uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ambao kukamilika kwake kutachochea ufanisi na kuleta tija katika kukuza Ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika ngazi ya uwili na kikanda na kimataifa.

Amewataka wafanyakazi wa wizara kuhakikisha ushirikiano, uhusiano na maelewano miongoni mwao huku wakiendelea kufanya kazi kwa weledi, ujuzi wa hali ya juu ili kuleta tija na ufanisi kwa taifa.

Pia amewapongeza wajumbe wa Baraza kwa kazi nzuri ya kuwawakilisha wafanyakazi wengine katika Baraza hilo.

Awali akizunguma kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema Wizara itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za Wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa tija na ufanisi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara, Bi Pili Sukwa amewaasa Watumishi wa Wizara kuendelea kutii sheria, kanuni taratibu na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Viongozi wa Wizara na Serikali kwa ujumla.

Mkutano huo, pamoja na mambo mengine umepokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na kupokea na kujadili Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kabla ya kuwasilishwa Bungeni.