Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Muheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuwa uelewa wa wananchi ni muhimu sana katika suala la Utawala Bora, hivyo APRM Tanzania ina dhima kubwa ya kuhakikisha kuwa wanajitahidi kuhamasisha umma ili uelewe hadhi ya Utawala Bora nchini.

Mhe Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar alipokutana na Taasisi ya Mpango wa hiyari wa kujitathimini katika vigezo vya Utawala Bora Afrika, Tawi la Tanzania.

Ameongeza kuwa APRM inayo dhima kubwa ya kutumia miongozo, Sera na nyenzo zote zinazostahiki ili kujenga uelewa mpana wa jamii katika utekelezaji wa dhana nzima ya Utawala Bora nchini ambayo ndio msingi muhimu kwa Maendeleo ya Taifa.

Na kwa upande wake Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Bw. Lamau Mpolo amesema kuwa APRM imejipanga kufanya Tathmini ya Pili ya masuala ya Utawala Bora Tanzania ili kuweza kubainisha yale mazuri yanayofanywa na Serikali na kuweza kuyaendeleza lakini pia kuibua changamoto zilizopo katika Jamii na kuchukuliwa hatua za kutatuliwa.

Ni vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikachagua Mtu/Taasisi maalum kwa Zanzibar ambayo itafanya kazi kwa karibu na APRM Tanzania ili kurahisisha zoezi hilo la Tathmini na kuweza kupatikana kwa nyaraka mbali mbali ambazo zitasaidia katika uandishi wa Ripoti hiyo na Zanzibar iweze kuonekana vizuri katika suala la Utawala Bora. Amesema Bw. Lamau

Nae Meneja Habari na Mawasiliano APRM Tanzania Ndg Badria Masoud amesema kuwa suala la Uhamasishaji kuhusu APRM na Ripoti ya Pili ya Tathmini ni jambo la kipaombele kwasasa hivyo APRM imejipanga kufanya kampeni kubwa ya Uhamasishaji ili kujenga uelewa kwa wananchi waweze kushiriki kutoa maoni yao na Tanzania ibaki kuwa kinara wa masuala ya Utawala Bora Afrika.