Mhe. Shigeki Komatsubara Mwakilishi Mkazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP-Tanzania) amesema kuwa Taasisi ya Mpango wa hiyari wa kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora (APRM Tanzania) ni miongoni mwa taasisi muhimu katika nchi ambazo zinalenga kukuza, kusimamia na kuendeleza masuala ya Utawala Bora.
Ameyasema hayo wakati alipokutana na uongozi wa APRM Tanzania katika Ofisi za UNDP Dar es Salaam mara baada ya kukamilishwa kwa utiaji saini wa hati ya makubaliano baina ya UNDP na APRM Tanzania.
Mhe.Shigeki amesema kuwa mpango wa APRM anaufahamu kwa muda mrefu ambao umekuwa Afrika katika suala la kubadilishana uzoefu kuhusu utawala bora, hivyo amefurahishwa sana na Tanzania kuwa ni miongozni mwa nchi waasisi wa mpango huu.
Ameielezea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi wananchama wa Mpango huu wa APRM tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003, ambapo APRM imekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya Taifa kwa kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi, kiutawala, utulivu wa kisisasa na mambo kadha wa kadha kwa mataifa ya Nje na yaliyoendelea haswa katika Uchumi wa Kidiplomasia.
Ameongeza kuwa Tanzania haina budi kufanya kazi kwa pamoja kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kutekeleza Agenda yake ya mwaka 2063 ikioanishwa na Agenda 2030 ya Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Bw. Lamau Mpolo alibainisha baadhi ya maeneo makuu ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo, ufahamu na utashi baina ya pande zote mbili kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa UNDP na APRM ni wa muda mrefu hivyo ni vyema kuuimarisha na kuuendeleza kwavile APRM ni chombo muhimu na ni kiungo cha Wananchi pamoja na Serikali yao katika shughuli zake za kuliletea maendeleo Taifa la Tanzania.
Mpolo amesema kuwa APRM ina jukumu kubwa la kuhamasisha dhana ya Utawala Bora kwa kutekeleza Sera, Viwango na Taratibu zitakazopelekea kuimarika kwa Siasa (Political Stability), kuongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi (High economic growth), uhakika wa maendeleo endelevu (Sustainable development), na kuharakisha mtangamano wa Kikanda na Bara zima la Afrika kwa nchi wanachama kwa kubainisha maeneo ambayo zinafanya vizuri ili kuyaimarisha pamoja na kubadilishana uzoefu.
Aidha ameongeza kwa kusema kuwa Mpango wa APRM unatekelezwa kwa kuzingatia misingi mikubwa mitatu ambayo ni kuzingatia Uwezo wa Kitaalam (Technical Competence), kundaa tarifa za uhakika na zenye kuaminika (Credibility) pamoja na uhuru wa kutotumika kisiasa (free from political manipulation).




